MWAKA UMEISHA, TUMEFIKIA MALENGO? | Bongo Voice
Breaking News
Loading...

Monday, December 30, 2013

MWAKA UMEISHA, TUMEFIKIA MALENGO?
MUNGU ni mwema sana. Ni bahati kubwa sana kwamba leo tumekuwa miongoni mwa watu ambao muumba wetu amewabariki kuwa hai na wenye afya njema, kwa sababu muda mchache tu uliopita, waliokuwa kama sisi hali zao zilibadilika ghafla, kwa wengine kufariki, kuugua na hata kujeruhiwa vibaya.
Huu ni ushahidi juu ya namna ambavyo Mungu ni wa ajabu sana na yatupasa kumshukuru na kumsujudia, kwani kwake yeye, kila jambo linawezekana.
Baada ya kusema hivyo, nirejee kwenye mada yangu ya leo. Saa sita usiku leo, tutakuwa tunamaliza siku 365 za mwaka 2013, mwaka ambao kwa kweli ulikuwa na pilika pilika nyingi sana kwetu kama taifa, jumuia na mtu mmoja mmoja. Mambo mengi yalitokea, kitaifa na kimataifa.
Siyo nia yangu kuzungumzia kila jambo lililofanywa au kufanyika, lakini angalau ingekuwa ni vyema tukiongelea vipaumbele vyetu kama taifa, jinsi tulivyoweza kukabiliana na changamoto zake, tulipofanikiwa na pale tuliposhindwa.
Mwaka unaomalizika leo ulikuwa na mambo mengi sana kwa taifa letu, kubwa hasa likiwa ni mchakato unaoendelea wa upatikanaji wa Katiba mpya. Tulishuhudia malumbano makali yakitokea bungeni ambayo kwanza yalilazimisha wabunge wa upinzani kususa kabla ya kukutana na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuweka sawa baadhi ya hoja zao.
Ni jambo la kufurahisha kwamba kwa masilahi ya taifa, wapinzani walikubali kurejea bungeni na kuendelea kuijadili rasimu hiyo kwa namna nzuri kabisa. Ni imani yangu kwamba mambo haya yatakwenda salama ili mradi mwisho wa siku, nchi yetu ndiyo iibuke mshindi wa katiba mpya, badala ya kuwa ushindi wa CCM, Chadema, CUF, UDP, NCCR-Mageuzi au chama kingine chochote cha siasa.
Lakini pia kulijitokeza hili suala la utekelezaji mbovu wa Operesheni Tokomeza Ujangili, ambayo ilisababisha mawaziri wanne kupoteza nafasi zao, baada ya kuibuliwa kwa malalamiko mbalimbali yaliyoambatana na uonevu, udhalilishaji, wizi, dhuluma, mauaji na hata mateso.
Wito wangu kwa mamlaka zinazohusika, ni vizuri kama haki ingetendeka kwa wote, waliouawa, kudhulumiwa, waliojeruhiwa na walionyang’anywa mifugo yao kufidiwa, sambamba na waliotenda maovu hayo nao kuchukuliwa hatua za kisheria, bila uonevu.
Taifa pia liliendelee na vita visivyoisha dhidi ya umasikini, ujinga na maradhi. Hali ya pato la Mtanzania mmoja mmoja iliendelea kudidimia, kwani suala la ukosefu wa ajira lilizidi, miundombinu mibovu iliendelea kuwa tatizo la kuzuia ubunifu mpya wa ajira kwa vijana.
Hali ya elimu bado ni janga la kitaifa. Watoto wa masikini walibaki kuwa waathirika wakubwa wa kutopata elimu bora, kwani uhaba wa walimu vijijini, vifaa na majengo bora ya shule, yalifanya mazingira kutokuwa rafiki kwa wanafunzi hao kufurahia masomo yao.
Huduma za afya nazo ziliendelea kuwa kikwazo kingine cha maendeleo kwa wananchi na taifa kwa jumla. Matibabu ya uhakika kwa watu wa kipato cha chini hayakuwa ya kujivunia hata kidogo na hili lilileta manung’uniko kutoka kwa walalahoi.
Hayo ni baadhi ya mambo ambayo kama taifa tunapaswa kuyazingatia wakati huu tukijiandaa kuingia mwaka mpya. Ni lazima utamaduni wa kuwajibika uanze kujengwa hivi sasa, kwani viongozi wetu wengi wameonekana kuendelea kufanya kazi kwa mazoea, jambo ambalo limekuwa likitugharimu sana.
Nimalizie kwa kuwasihi tena viongozi watendaji wetu. Mungu ametubariki kuwa na kila kitu cha kutuwezesha kuachana na umasikini tulionao, tatizo letu ni moja tu, nalo ni la wakubwa wetu kutokuwa na uzalendo na kuliingiza taifa katika matatizo ya kiuchumi.
Tunakosa uzalendo tu, vinginevyo leo hii tungekuwa mbali kimaendeleo.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli!

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT

 

Google+ Badge

Google+ Followers