MAPENZI BILA NDOTO NI WIZI MTUPU | Bongo Voice
Breaking News
Loading...

Sunday, January 5, 2014

MAPENZI BILA NDOTO NI WIZI MTUPU

MAPENZI ni maisha ya kawaida ambayo wawili wanaotamkiana kupendana wanaishi. Kutamkiana kwa sababu si kila kitokacho kinywani kinaweza kuwa na maana ileile ya moyoni. Dhana nzima ya mapenzi haina urafiki na maigizo. Waigizaji hufeli katika kipengele cha uhusiano.
Usipoteze muda wako na mtu ambaye moyo wako unamkataa. Kama kweli unampenda basi acha mawenge, mpe kila anachostahili, maana huyo ndiye wako wa maisha. Mara nyingi mpenzi bora haji kama zawadi kwamba utamkuta na sifa zote unazozihitaji.

Hutokea kukutana na mwenzi ambaye unamkubali kutokana na muonekano wake wa juu lakini baada ya kukaa naye kwa muda ndipo utaanza kumbadilisha mpaka kukidhi sifa ambazo wewe unazikubali. Upo msemo “ukiona vyaelea jua vimeundwa”, utumie kuujenga uhusiano wako.
Unaweza kumfanya mwenzi wako mkorofi kuwa mnyenyekevu kama tu utaamua kumbadilisha katika lugha ya upendo. Nimezungumzia lugha ya upendo kwa sababu ukiwa mzuri wa kutoa maneno makali hutamsaidia mpenzi wako kubadilika, zaidi ukali wako ni sawa na kuzidi kumfanya awe ovyo.
Kitendo cha watu kushindwa kuwatengeneza wapenzi wao ndiyo zao la migogoro mingi kutawala kwenye uhusiano wa wengi. Zipo sababu nyingine kama vile kuvumiliana, kutotambua thamani ya mpenzi lakini kubwa zaidi kutokuwa na ndoto.
JE, UNAAMINI KATIKA NDOTO?
 Wengi wanaingia katika uhusiano wa kimapenzi wakiwa hawana ndoto. Kwanza hawajui ni kitu gani, kwa hiyo hawaheshimu. Hili ni tatizo la kimsingi kabisa kwenye uhusiano wa watu wengi. Kabla hujaanza safari ya kimapenzi, jiulize “je, nina ndoto na huyu niliye naye?”
Makosa mengi yamekuwa yakitendeka katika eneo hili. Mtu anaanzisha uhusiano na yule ambaye hana ndoto naye. Matokeo yake yanakuwa ni migongano na kutotimia kwa malengo ya wahusika. Kuwa na mpenzi ambaye huna ndoto naye ni sawa kumpigia mbuzi gitaa, ukiamini atasikia muziki na kuucheza.
Pengine wewe ndani yako unaona ndoto juu yake lakini yeye hana. Hapa namaanisha kuwa usiishie tu kujitambua wewe binafsi kuwa una ndoto na yeye, badala yake akili yako uishughulishe kutafuta ukweli ndani yake unaokuhusu. Ukishagundua kwamba hana ndoto na wewe, chukua hatua haraka.
Wengi walichukuana, wakajitahidi kuyajenga maisha pamoja lakini hawakufika popote. Inawezekana hata mke na mume kuingia kwenye ndoa lakini bado ikawa hakuna matunda chanya. Ukiona ndoa ina misuguano miaka nenda rudi, chunguza halafu utagundu kuwa wahusika hawakuwa na ndoto.
Mke na mume wanakuwa na balaa la usaliti! Mke anachepukia kule, mume anajirusha kivile. Kama wahusika wangekuwa na ndoto za kuishi pamoja, halafu ndoto hiyo ndiyo ingetumika kuwafanya wachumbiane kabla ya kuoana, heshima ingekuwepo.
Usaliti, ukosefu wa uvumilivu, kutoheshimiana na mambo mengine kama hayo, ni matokeo ya kukosekana kwa ndoto baina ya wawili waliotamkiana kuwa wanapendana.
GPL

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT

 

Google+ Badge

Google+ Followers