TANESCO YACHARUKA | Bongo Voice
Breaking News
Loading...

Wednesday, January 15, 2014

TANESCO YACHARUKA

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limeanzisha operesheni maalumu ya kukusanya madeni yanayofikia Sh bilioni 233, ambapo wateja watakaokaidi zikiwamo taasisi za umma na binafsi, zitakatiwa umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Felchesmi Mramba alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 129 ni za taasisi za Serikali ikiwamo Zanzibar inayodaiwa Sh bilioni 70 na Sh bilioni 104 watu, taasisi binafsi na viwanda.
“Kwa sasa shirika limeanzisha kampeni maalumu ya kukusanya madeni itakayojumuisha kutoa notisi ya kutaka wateja kulipa ndani ya muda huo na kuwakatia wote ambao hawajalipa.
“Tunawataka wateja wote walipe madeni yao mapema iwezekanavyo ili kuepuka usumbufu,” alisema.
Kukatika umeme Mramba pia alikiri kutokea kwa hali ya kukatika umeme katika baadhi ya maeneo ya nchi hasa Kanda ya Ziwa na baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam hasa Ubungo na katikati ya Jiji hivi karibuni.
Akielezea hali hiyo, alisema ilisababishwa na hitilafu za mtambo zilizotokea katika vituo vya Sokoine na Ubungo, Dar es Salaam pamoja na kuanguka kwa nguzo kubwa mbili za vyuma wilayani Kahama.
Alifafanua, kuwa Ubungo kulitokea wizi wa nyaya za shaba za ambazo inaaminika wezi hao huziuza kama chuma chakavu.
Kwa upande wa Kahama, kulitokea wizi wa vyuma ambavyo wezi huvitumia kutengeneza mikokoteni ya kukokotwa na ng’ombe na majembe ya kulimia ya plau.
“Tumepata hasara kubwa ya Sh bilioni 1.2 Kahama na Sh milioni 200 Ubungo.
Tunatoa rai kwa Watanzania kujali miundombinu ambayo ni rasilimali ya Taifa na kuepuka vitendo vinavyoleta usumbufu kwa Watanzania wenzao, kusababisha hasara na kurudisha nyuma hatua kubwa za maendeleo zilizokwishapigwa,” alisema.
Umeme wa mafuta Kuhusu hali ya uzalishaji umeme, Mramba alisema ni ya kuridhisha na hakuna upungufu wa umeme pamoja na mahitaji ya huduma hiyo kuendelea kuongezeka.
Hata hivyo, alibainisha kuwa bado Tanesco inaendelea kutumia mitambo ya mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura ambao ni ghali, ili kukidhi ongezeko la mahitaji linaloendelea. Mahitaji ya umeme kwa sasa kwa mujibu wa Mramba ni megawati 898 tofauti na ilivyokuwa mwaka jana, ambapo mahitaji yalikuwa megawati 851.
“Hii imelazimu kuzalisha umeme zaidi ili kukidhi mahitaji haya ya ziada. Ni muhimu kufahamu kuwa kiasi kikubwa cha uzalishaji kinatokana na mitambo ya mafuta,” alisema.
Alielezea uwiano wa mchango wa mitambo hiyo katika kukidhi mahitaji, kwamba mitambo ya mafuta, ambayo ndiyo ghali zaidi, inatoa asilimia 45 ya umeme unaozalishwa.
Mitambo ya gesi ambayo ni ghali pia lakini si kama ya mafuta, inatoa asilimia 42 ya umeme huo, huku mitambo ya maji ambayo ndiyo inayotoa umeme kwa gharama nafuu zaidi, ikichangia asilimia 13 tu ya mahitaji ya umeme nchini.

Rekodi ya wateja Katika hatua nyingine, Tanesco imevunja rekodi ya kuunganishia umeme wateja 143,000 mwaka jana, idadi ambayo haijawahi kufikiwa tangu kuanzishwa kwa shirikia hilo.
Hata hivyo, Mramba alisema bado kuna maombi mengi hayajafanyiwa kazi, lakini akaahidi kuwa wateja wote walioomba kuunganishiwa umeme mwaka jana, watahudumiwa kwa kasi na ifikapo Februari wataanza kupata huduma hiyo.
“Tutaendelea kuwaunganishia umeme kwa kasi kama tulivyoahidi ili ifikapo mwishoni mwa Februari tuwe tumewaunganishia. Vifaa vinaendelea kuwasili na kazi zinaendelea vizuri,” alisema Mramba. Ili kuendeleza kasi hiyo, alisema Tanesco itabadilisha utaratibu wa ununuzi wa vifaa ili kuondokana na matatizo ya mara kwa mara ya uhaba.
“Hii itajumuisha ununuzi wa vifaa kwa wingi mikoani ili kupunguza mlundikano wa majukumu yanayofanyika makao makuu,” alisema. Hujuma mitandaoni Mramba pia alielezea masikitiko yake kutokana na kuibuka kwa baadhi ya watu wanaohujumu shirika hilo katika mitandao ya mawasiliano nchini.
Kwa mujibu wa Mramba kuna akaunti za mtandao wa twitter zilizoanzishwa na baadhi ya watu zinazodaiwa kuanzishwa na Tanesco. “Twitter hizi zimekuwa zikitumika kuchafua shirika na kukejeli wateja.
Majina yake ni Tanesco@TANESCO-, TanescoEscobar@tanescobar na TANESCO LTD-@tanesco-,” alisema.
Alisema wameiharifu Mamlaka ya MawasilianoTanzania (TCRA) na Jeshi la Polisi, ili wachukue hatua stahiki kwa mitandao ya kijamii inayotumika kulichafua shirika hili kwa kufungua akaunti kwa kutumia jina la Tanesco.
CHANZO HABARI LEO

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT

 

Google+ Badge

Google+ Followers