WAZIRI MKUU MSTAAFU LOWASSA ALIPOFUNGUKA BUNGENI LIVE!!

HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA EDWARD LOWASSA (Mb), WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA TANO WA BUNGE, DODOMA TAREHE 15 NOVEMBA, 2006
 
Mheshimiwa Naibu Spika, tunakaribia mwaka mmoja tangu Serikali ya awamu ya nne iingie madarakani Desemba, 21, 2006. Watanzania wengi naamini wameona juhudi za Viongozi wao katika kushughulikia matatizo mbalimbali ya kijamii. Lakini wapo pia wenye mashaka. Katika gazeti la Mtanzania toleo Na. 3838 la tarehe 10 Novemba, 2006 mshairi Emmanuel Marwa (Msemakweli – Mbiu ya Ushairi) wa Dar es Salaam anauliza kama viongozi wenye kujali maslahi ya wananchi wapo nchini. 
Kwa maneno yake anasema ifuatavyo:
1. Wako wapi maridadi, viongozi mashujaa,
Wanaotimiza ahadi, wanyonge kuwakomboa,
Wasafi si mafisadi, weupe waso na waa.

2. Wako wapi wenye nguvu, wavumao kama radi,
Walinzi wakakamavu, wakeshao kama bundi,
Wapingao uonevu, na kuchapa magaidi.
3. Wako wapi manabii, wahubirio ukweli,
Wanaoenzi uhai, kukemea ukatili,
Marubani wa jamii, wenye dira na adili.
4. Wako wapi waungwana, wakunga wenye huruma,
Wazuri waso hiana, wachukiao dhuluma,
Wanaoheshimu dhamana, wajibu wao kwa umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu hawa wananikumbusha hadithi aliyotusimulia Rais Mstaafu, Mheshimiwa Benjamin Mkapa ya walevi wawili waliokuwa wanatembea usiku. Mmoja akaangalia juu, akamwambia mwenziwe, “Usiku wa leo ni mzuri kweli. Hebu ona mwezi ulivyopendeza!” Mwenziwe akasimama, akapepesuka kidogo, kisha akajibu, “Wewe vipi, umelewa nini? Huo sio mwezi, hilo ni jua”. Wakabishana kwa muda mpaka walipomuona mtu wa tatu akipita karibu yao. Kumbe naye mlevi. Wakamuliza, “Samahani bwana. Hebu tusaidie. Lile ni jua au ni mwezi?” Mlevi wa tatu akasimama, akafinya macho, kisha akajibu, sijui bwana nami ni mgeni hapa!”.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumthibitishia mshairi na Watanzania kwa ujumla kuwa viongozi wanaoulizwa wapo nchini. Tena wamejaa tele. 
Niruhusuni nimjibu
Bwana Marwa kwa beti zifuatazo:-

Tupo tumejaa tele, viongozi mashujaa,
Tupo mstari wa mbele, vyema tumejiandaa,
Twatenda bila kilele, katu hatukuzubaa,
Tupo tumejaa tele.

Tupo tulioadilifu, tuso doa wala toa,
Tusoyapenda machafu, matendo yaso murua,
Twakemeya uhalifu, ufisadi na hadaa,
Tupo tumejaa tele.

Tupo tupendao watu, kwa huba na kuwajali,
Tunaothamini utu, na kupinga idhalali, 
Dhuluma ni mwiko kwetu, haki hushinda batili,
Tupo tumejaa tele.

Tupo tulo waungwana, viongozi majasiri,
Wenye mipango mwanana, iliyopangwa vizuri,
Yenye tija na maana, ya fursa kwa mafakiri
Tupo tumejaa tele.

Mheshimiwa Niabu Spika, mafanikio ya mkutano wowote wa Bunge huwa ni matokeo ya ushirikiano wa wadau wengi. Hata hivyo, bila uongozi wako thabiti, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti, mafanikio hayo yasingepatikana.

 

Tumeweza kukamilisha kazi zote zilizopangwa. Aidha, nakushukuru kipekee Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge ambao kwa muda wote wameonyesha kuzielewa kanuni na taratibu za kuliongoza Bunge kila walipopewa nafasi kutuongoza. Wote nawapongeza sana. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushauri wenu wa mawazo wakati wa kujadili miswada na maazimio tuliyo pitisha katika mkutano huu. Lakini nawapongeza pia Mawaziri waliowasilisha Miswadwa na hasa Mheshimiwa Mizengo K. P. Pinda mlie mbana sana jana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Namshukuru Katibu wa Bunge, Bw. Daniel Foka na Wafanayakazi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kutuwezesha kukamilisha shughuli zote zilizopangwa bila matatizo.

Nawashukuru watumishi wa Serikali na taasisi zake kwa kuiwezesha kutekeleza wajibu wake ipasavyo. Aidha, navishukuru vyombo vyote vya habari kwa kuonyesha dhahiri kuwa bila wao kuwepo, wananchi hawawezi kuelewa kinachoendelea ndani ya ukumbi huu. 
 Sasa nawaomba Waheshimiwa Wabunge:

• Twendeni tukasimamie ujenzi wa madarasa ya wanafunzi wapya wa Sekondari.
• Twendeni tukasimamie uanzishaji na uimarishaji wa SACCOS.
• Twendeni tukasimamie miradi ya TASAF.
• Twendeni tukasimamie mikopo tuliyoitangaza iwafikie walengwa.
• Twendeni tukasimamie kilimo kwa mvua zinazoanza.
• Twendeni maana sisi ndio viongozi na sisi ndio tunaweza. Tunaweza –Twendeni!


Mheshimiwa Naibu Spika
, leo ni tarehe 15 Novemba, 2006. Katika kipindi cha mwezi mmoja na nusu tutakuwa tumefikia mwisho wa mwaka 2006. Ni matumaini yangu kwamba inshallah Mwenyezi Mungu atatujalia sote tuweze kumaliza mwaka salama. Napenda kutumia fursa hii kuwatakia nyote Krismas Njema na Kheri ya Mwaka mpya!

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya naomba kutoa hoja kwamba,Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 30 Januari, 2007 Jumanne saa 3.00 asubuhi, litakapokutana hapa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
WAZIRI MKUU MSTAAFU LOWASSA ALIPOFUNGUKA BUNGENI LIVE!!  WAZIRI MKUU MSTAAFU LOWASSA ALIPOFUNGUKA BUNGENI LIVE!! Reviewed by Linnah Lsquare on 11:13 AM Rating: 5
Powered by Blogger.