Hawataki kukosolewa....

Kuna ukweli kwamba, mwanaume ana namna tofauti ya kuyatazama na kuyakabili mambo, hasa anapokuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi. Kwa mfano, mwanamke anapokuwa maarufu, ni hatari sana kwake kujaribu kuutumia umaarufu wake katika kumshusha mumewe. Lakini, hata jaribio la kumwonesha mumewe kwamba, yeye ni zaidi yake ni kosa kubwa.

Ni kosa kubwa kwa sababu kwa asilimia ya kutosha wanaume wanawaogopa wanawake, ‘smart’ siyo hapa kwetu tu, bali hata Ulaya na Marekani. Kwenye tafiti fulani za hivi karibuni katika nchi za Ulaya na Marekani ilibainika kwamba, wale wanawake wenye kuonekana kuwa wanajua mambo mengi kuliko wanaume, wanaolewa kwa shida sana ukilinganisha na wale ambao, hawajui au wanajifanya kwamba, hawajui mambo.

Tafiti hizi zinaonesha kwamba, kwa kadiri mwanamke anayokuwa na uwezo zaidi wa kiakili, kulinganisha na wanaume wengi, ndivyo jinsi nafasi yake katika kuolewa inavyopungua kwa wastani wa asilimia 40.

Utafiti uliowahi kufanywa na chuo kikuu cha Michigan huko nchini Marekani, ulionesha kwamba, wanaume huamini kwamba, mwanamke ‘smart’ anakuwa kwenye nafasi nzuri ya kufanikiwa. Kwa wanaume, mafanikio ya mwanamke hasa kazini, yana maana ya mwanamke huyo kuwa katika nafasi ya kuzini sana. Unaona ilivyo eh..!

Ukweli ni kwamba, wanawake wengi kiasi cha kutosha walio ‘smart’ huathiriwa sana na mitazamo ya wanaume, pale inapotokea kwamba, mwanamke anaingia kwenye mafanikio ya kipato, yu mjanja zaidi au ana uwezo mkubwa kiakili kuliko mwanaume. Lakini cha ajabu ni kwamba, idadi ya wanawake wanaowazidi wanaume kimali na kiakili inazidi kuongezeka kila uchao.

Haiyumkini hiyo ndio sababu kuna idadi kubwa ya wanawake wenye mafanikio ambao wamezalishwa na kutelekezwa na wanaume, huku ndoto zao za kuolewa na kujenga familia zikionekana kuwa ngumu kutimia.

Kwa bahati mbaya sana wanawake hawa hawafanikiwi kwenye matarajio yao ya kuolewa kwa sababu akilini mwa wanaume kuna kitu tofauti kinatembea humo. Kuna kitu chenye kuwaambia kwamba, mwanamke ‘smart’ hafai kabisa kuolewa……!