JIFUNZE UMUHIMU WA SUBIRA KATIKA MAFANIKIO NA MAHUSIANO!!!

Hata katika kuelekea kujenga uhusiano imara kunahitaji subira.....


Ralph Waldo Emerson, mkongwe wa ufahamu, aliwahi kusema. Fuata mwenendo wa maumbile, siri yake ni subira. Subira hiyo yaweza kukufikisha kwenye maisha bora kama unajua jinsi ya kufanya kazi na Nguvu ya Subira na maumbile kwa pamoja.

Kwa nini subira ni ya lazima kwa mafanikio?

Muulize mfanyabiashara yoyote aliyefanikiwa ama yeyote aliyefanikiwa bila ujanjaujanja, atakwambia kwamba, hakufikia uamuzi mara moja. Huchukua muda mrefu wa utafiti, kufuatilia na kufikiria, wakisubiri hadi muda muafaka kufanya uamuzi. Maumbile hufanya kazi kupitia mchakato maalum na yana uwezo mkubwa wa kusubiri.

Kwa mfano: Unataka kupanda mbegu, imwagilie maji, iache kwa muda, na utakapofikia muda muafaka, wakati kila kitu kiko sawa, mbegu hiyo itaanza kuota na baadaye mmea. Hii ni kwa mmea wowote utakaoupanda. Hii hutokea tu wakati hali inapokuwa sawa, lakini kulikuwa na kazi iliyokuwa ikiendelea kufanywa kabla ya matokeo yote haya kuchukua nafasi yake. Mbegu inatakiwa kupandwa, inatakiwa kutunzwa, inatakiwa kuachwa ili ianze kutoa mizizi michanga ardhini, na baadaye muda utakapofika mmea unaanza kujitokeza juu ya ardhi katika hali hasa iliyotarajiwa. Bila kuweko kazi ya mwanzo ya kupanda na kumwagia maji mbegu, mmea usingetokeza juu ya ardhi, na hungeweza kuwa na bustani yako ya matunda ama maua ambayo huenda hivi sasa unakula matunda yake.Kama unataka kufikia malengo yako, iko haja ya kuwa na subira ya aina hiyo. Hii haina maana kwamba ukae kitako na kusubiri kila kitu kiende kwa wakati wake. Badala yake unatakiwa kufanya kazi kwanza, kuweka msingi, kupanda mbegu, na kuhakikisha ardhi unayolima ni ya kufaa. Tayarisha na usubiri kwa kila hali kuwa sawa kabla ya kutoa maamuzi sahihi yatakayokusukuma kwenye mafanikio makubwa. Kwa bahati mbaya, watu wengi hawako tayari kufuata mchakato huu na badala yake wanataka kwa siku moja kupata kila kitu katika maisha yao. Siyo wazuri kufuata taratibu zinazokubalika za vitu kubadilika, na hivyo hujikuta wakitaka vitu vibadilike mara moja na hivyo kuishia wakichanganyikiwa na kukata tamaa kutokana na mabadiliko haya ya ghafla kushindikana.

Moja kwa moja hiyo huwa haifanyi kazi. Wakati unapofanya kazi kinyume cha maumbile, unasukumwa nyuma zaidi. Ikiwa unataka kufanikiwa, unatakiwa kuwa na subira kwa kiasi fulani. Fikiria kile unachotaka ufanikisha, fikiria kuhusu mabadiliko unayoyataka, anza mchakato wa kuleta mabadiliko haya kwa kujua kile unachotaka na kwa nini. Pandikiza mbegu zako za mafanikio kwenye bustani ya akilini mwako. Kuwa na subira ukisubiri alama za nyakati za kukuruhusu kuendelea. Hakikisha mawazo yako ya kawaida na yale ya kina yanafanya kazi kwa pamoja ili kukusaidia kufikia malengo yako. Wakati unapokosa subira, wakati unaposhindwa kuamini na kukubali kwamba mambo yatakuwa, huwa unapunguzwa kasi yako, kukwamishwa na hatimaye kuishia kwenye njia isiyo sahihi na baadaye unashangaa:
‘Nimefika vipi hapa?’

Kwa mfano, uko kwenye foleni ukisubiri kulipia kitu fulani, foleni ni ndefu, lakini kuna mtunza fedha mwingine ambaye naye ana foleni ndefu kama hiyo. Kama utachoka na kukasirika, haitakusaidia. Ikiwa utaamua kuhamia mstari mwingine, hiyo huenda ikakuchukua muda mrefu zaidi, kama utaacha na kuondoka, hutopata kile unachohitaji. Unaweza kuamua kuondoka ukipanga kurudi foleni itakapopungua, lakini baadaye ama ukashindwa kurudi ama unaporudi ukakuta foleni ni ndefu maradufu ya ile ya kwanza na hivyo kuamua kuachana kabisa na zoezi hilo ulilotaka kulifanya, na hivyo kukosa kile ulichotaka.

Unapokosa subira unakasirika haraka, ukidhani mambo ni rahisi upande wa pili, lakini ukaondoka bila kupata kile unachotaka. Kama ungekuwa na subira, ungeweza kufanya malipo yako na kuendelea na kile ulichotaka. Usifikirie mambo ni mazuri upande wa pili, shughulika na kile ulichonacho na kile unachojua na hivyo kuwa na subira na utatoa maamuzi sahihi
. Ukikimbilia Marekani kwa kudhani huko mafanikio yanakuja mara moja, utashangazwa. Utakaa huko kwa miaka kumi na ukirudi hapa nchini, utakuta uliyemwacha akiwa anafanya kile ulichoona hakilipi, akiwa mbali sana.

Ni vigumu mtu kuanza na kufanikiwa kupata fedha nyingi katika kipindi kifupi kama cha miezi mitatu, kwa sababu lazima zitakuwepo taratibu zinazohitaji kufanyika kama ilivyo kwa wakati wa kupanda mbegu. Ikiwa utakuwa na subira na kungojea mchakato ufikie wakati wake, ni wazi utapata mamilioni ya fedha si kwa miezi mitatu tu, bali katika kipindi kirefu cha maisha yako, mpaka pale utakapokiuka mchakato wake. Unaweza kujaribu kufanya mambo ya haraka kwa kujaribu mradi na hivyo kuwekeza kwenye miradi ya hatari na pengine kuishia kuingia kwenye uchezaji wa kamari na bahati nasibu, lakini ni wazi utapoteza fedha nyingi zaidi. Hata unapoyatazama maisha ya binadamu, utakuta yanafanya kazi kwa kufuata utaratibu wa maumbile, utaratibu wa kusubiri.

Tunaanza tukiwa watoto wadogo, tunakuwa, na kuwa watu wazima na umri unazidi kupanda hadi kuzeeka, kama ilivyo kwa utaratibu wa maumbile. Mtu hawezi kuzaliwa leo na kufikia umri wa utu uzima ili aweze kuwahi nafasi fulani ya kazi ambayo hivi sasa iko wazi. Mafanikio katika maisha huwa hayatokei kwa usiku mmoja. Kuanzisha biashara na kuifanya ifanikiwe kunahitaji subira. Kukosa subira katika biashara ni kualika janga. Uhusiano nao huchukua muda kuujenga na kuuboresha, kukosa subira katika uhusiano ni njia fupi ya kuhitimisha uhusiano huo. Kutafuta kazi sahihi kunahitaji subira na juhudi, kukosa subira katika kutafuta kazi ni njia rahisi ya kuikosa kazi hiyo. Mambo yanaweza kutokea ghafla, lakini mafanikio yanahitaji subira. Kwa mfano, waweza ukakutana na mwenza wako hata leo, lakini mafanikio ya uhusiano wenu huo yatahitaji subira ili yaweze kukua na kufanikiwa.

Unaweza ukawa na wazo la biashara hata leo, lakini kwa biashara hiyo kuweza kukua hadi kufikia mafanikio kutategemea jinsi utakavyokuwa na subira si kwa kazi tu, bali pia kwa wafanyakazi wenzako na viongozi wako. Ili kuanza kujenga msingi wa mafanikio yako leo, anza kupanda mbegu hivi sasa ili uweze kupata mafanikio yako hapo baadaye.

JIFUNZE UMUHIMU WA SUBIRA KATIKA MAFANIKIO NA MAHUSIANO!!! JIFUNZE UMUHIMU WA SUBIRA KATIKA MAFANIKIO NA MAHUSIANO!!! Reviewed by Linnah Lsquare on 6:04 AM Rating: 5
Powered by Blogger.