MABOSI TBS, ATCL WAKAANGWA KORTINI!! | Bongo Voice
Breaking News
Loading...

Wednesday, February 5, 2014

MABOSI TBS, ATCL WAKAANGWA KORTINI!!

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
MABOSI wa zamani wa mashirika ya umma, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), jana walipanda kizimbani kujibu mashitaka yanayowakabili kutokana na uamuzi waliofanya walipokuwa wakiongoza mashirika hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Joseph Masikitiko, aliieleza mahakama kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Charles Ekelege, alitoa msamaha wa ada ya utawala kwa kampuni mbili bila kufuata taratibu.
Masikitiko alidai hayo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh milioni 68, inayomkabili Ekelege.
Ekelege anadaiwa kusababisha hasara hiyo baada ya kuondoa ada ya asilimia 50 ambayo ni sawa na Sh milioni 68, kwa Kampuni za Jaffar Mohamed Ali na Quality Motors bila idhini ya Bodi.
Akiongozwa na Wakili Janeth Machulya kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Masikitiko alidai kuwa anazifahamu kampuni hizo kwa kuwa zilikuwa zinafanya kazi ya ukaguzi wa magari kutoka nje kwa niaba ya TBS.
Alidai katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2009 akiwa Meneja wa Fedha na Utawala, hajawahi kupokea wala kushughulikia barua za maombi ya kuondolewa kwa ada ya utawala kutoka kampuni hizo mbili.
Kificho
Aidha alidai hakujua kama kampuni hizo zilipewa msamaha wa ada, hadi alipopata ripoti ya ukaguzi wa hesabu za nje ya mwaka 2008 hadi 2009, na kusikia kwenye kikao cha Baraza la Utendaji ambalo kwa sasa ni Bodi ya Wakurugenzi, cha Septemba 30 mwaka 2011.
Alidai katika kikao hicho yeye akiwa mualikwa, walipata taarifa kuwa Menejimenti ilitoa msamaha wa ada hiyo bila kupata kibali cha bodi hiyo, ambapo bodi iliona walitoa msamaha huo kimakosa na kuwaonya wasirudie tena.
Alidai taratibu za kuomba msamaha wa ada ni kuwasilisha barua kwa Mkurugenzi, kisha iende kwa Mhasibu Mkuu atakayeandika dokezo kwa Mkaguzi wa Ndani ambaye ataangalia kama amekidhi vigezo vya kusamehewa, itapelekwa kwa Meneja wa Fedha kisha Mkurugenzi ataipeleka Bodi ya Wakurugenzi kwa ajili ya kuidhinishwa.
Akihojiwa na Wakili Majura Magafu anayemtetea Ekelege, Masikitiko alidai kuwa, Bodi haikusema kama Ekelege alifanya kosa, bali ilisema Menejimenti ilifanya makosa kwa kutoa msamaha huo bila kupata kibali.
Inadaiwa kuwa Machi 28, mwaka 2008 na Agosti 7, mwaka 2009, Ekelege alitumia madaraka vibaya na kusamehe ada kampuni mbili kwa asilimia 50, ambayo ni sawa na Sh milioni 68 bila idhini ya Baraza la Utendaji kinyume na utaratibu wa TBS pia alilisababishia shirika hilo hasara ya fedha hizo.
Mataka
Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya Kuhifadhi Magari Yanayodaiwa Kodi, Bartholomew Kijazi, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa wanalidai Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) Sh milioni 206.4.
Kijazi alidai hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kutumia vibaya madaraka kwa kutangaza zabuni na ununuzi wa magari chakavu 26, inayomkabili Mkurugenzi wa zamani wa shirika hilo, David Mattaka na wenzake wawili.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Shedrack Kimaro, Kijazi alidai kuwa wanaidai ATCL fedha hizo kutokana na kuhifadhi magari tisa katika ghala lao lililopo Mbagala, tangu 1998 hadi Novemba mwaka jana.
Alidai kuwa Desemba 16, 2011 aliandaa ripoti ya mtiririko wa kuingiza na kutoa magari 26 ya kampuni ya ATCL pamoja gharama za kuhifadhi na kukarabati, baada ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuomba ripoti hiyo.
Alidai wakati huo walikuwa wanaidai ATCL dola za Marekani 118,000 kutokana na kuhifadhi magari hayo kwa miezi 39 kwenye ghala lao la Mbagala, ambapo kati ya magari hayo, magari 15 yalitolewa na mengine tisa yamebaki kutokana na kukosekana kwa fedha za kulipa ushuru wa forodha.
Alifafanua kuwa kwenye ghala lao wanatoza kila gari dola 250 kwa mwezi na hadi kufikia Novemba mwaka jana, walikuwa wakidai shirika hilo dola za Marekani 129,000 ambayo ni sawa na Sh milioni 206.4.
Alidai ATCL walihifadhi magari hayo katika ghala lao kuepuka gharama za bandarini ambapo kwa siku wanatoza dola za Marekani 25 hadi 40 kulingana na ukubwa wa gari na kwa mwezi ingekuwa dola 1,200.
Mbali na Mattaka washitakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Elisaph Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani, William Haji.
Washitakiwa wanadaiwa kula njama, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya dola 143,442.75 za Marekani kwa kuagiza magari 26 chakavu kwa gharama ya Dola 809,300 kutoka Kampuni ya Bin Dalmouk Motors ya Dubai bila kutangaza zabuni ya ushindani.
Aidha wanadaiwa kuruhusu kununuliwa kwa magari hayo bila mkataba wa ununuzi ambao umewekwa saini na wahusika na kuthibitishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuisababishia Serikali hasara baada ya kushindwa kulipia kodi na kuchukua mkopo kwa ajili ya kuyakomboa na kuyatunza.
CHANZO HABARI LEO

google+

linkedin

0 comments:

POST A COMMENT

 

Google+ Badge

Google+ Followers