MWANAUME AJINYONGA...

Na Waandishi Wetu
NI simulizi ya majonzi! Fundi seremala Samuel Masanja,  mkazi wa Ilala jijini Dar amechukua ‘maamuzi’ magumu ya kujinyonga hadi kufa kwa kile kinachodaiwa kuwa ni msongo wa mawazo kwa sababu ya madeni yaliyosababishwa na kuwepo kwa uhusiano wake na kimada mmoja.
Marehemu Samuel Masanja enzi za uhai wake.
Kwa mujibu wa mtu wa karibu na marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Stany, kipindi cha uhai wake Samuel hakuwa na maelewano mazuri na mkewe kisa kikidaiwa ni mkewe kugundua mumewe ana kimada jirani na makazi yao.
Ilidaiwa kuwa, uhusiano wa marehemu huyo na kimada wake ulisababisha kuibuka kwa madeni likiwemo la kuwekeza kwenye mradi wa kuku na biashara kuyumba.
“Marehemu aliwahi kunieleza kwamba mambo ya wanawake zake yalimuumiza kichwa maana mkewe alikereka na kitendo cha kuwa na hawara huku kimada naye akipanga mambo yenye matumizi makubwa ya pesa kiasi cha kumfanya akopekope,” alisema rafiki huyo.
Akizungumza na gazeti hili juzi nyumbani kwake, mke wa marehemu Samuel, Hazina Mbaga ambaye ameachiwa jukumu la kulea watoto watatu, Beatrice, Happy na Timo alisema:
“Mpaka siku za mwisho za uhai wake, marehemu alikuwa akinilalamikia kuhusu wimbi la madeni aliyokuwa nayo na alionesha anajutia kitendo cha kuwa na kimada.
“Mwezi wa kumi mwaka jana, marehemu alitoweka nyumbani na kuanza kuonekana kwa nadra. Ni  baada ya kumpata huyo mwanamke wa nje.
“Alikuwa haleti matunzo ya watoto hata pale alipoitwa serikali ya mtaa baada ya mimi kwenda kumshtaki ingawa aliwahi kuniambia wazi kwamba, huyo mwanamke amekuwa akimkosesha muelekeo wa maisha lakini hawezi kumuacha.
“Siku anakumbwa na mauti alinifuata na kuniambia kwamba ameamua kurudi nyumbani moja kwa moja na kuachana na kimada wake, lakini akaniomba niitunze familia.
“Alisema ya dunia yamemshinda hivyo anaamua kurudi nyumbani. Mimi nikajua nyumbani tunapoishi maana alinifuata sehemu ya biashara. Alipoondoka, baadaye nikasikia amejinyonga nyumbani.”
Kwenye suruali yake ilikutwa barua yenye ujumbe uliosomeka: “Ya dunia yamenishinda kutokana na masuala ya madeni ni bora nikapumzike kuzimu.”
Juhudi za kumpata kimada huyo ziligonga mwamba baada ya kudaiwa kuingia mitini.

MWANAUME AJINYONGA... MWANAUME AJINYONGA... Reviewed by Linnah Lsquare on 11:30 PM Rating: 5
Powered by Blogger.