MAZITO YAIBUKA KUHUSU MJENGO WA KIFAHARI WA DIAMOND

WAANDISHI WETU
SIKU chache baada ya sehemu ya ukuta wa uzio wa mjengo wa msanii nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ kuanguka, mtaalam wa majengo aliyejitambulisha kwa jina la Injinia Stuart Daniel ameupiga zengwe akidai licha ya kuonekana kuwa na nakshinakshi nyingi, lakini ni dhaifu na unaweza kudondoka.
Sehemu ya ukuta wa nyumba ya msanii nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’ iliyobomoka.
Akizungumza na Gazeti la Amani mwanzoni mwa wiki hii  baada ya nyota huyo kutupia picha za uzio wake katika mtandao  ukiwa chini kwa mwereka wa mvua, Injinia Stuart alisema anaamini nyumba ya Diamond imejengwa chini ya kiwango na mafundi walimchakachua simenti.
MSIKIE MWENYEWE INJINIA
“Kama jengo lote lilijengwa kwa staili hii, basi ni suala la kusubiri kwa muda tu kabla hatujasikia habari za kuanguka kwake na kama hatakuwa makini, linaweza kumletea madhara makubwa. “Kitu ambacho ningeweza kumshauri ni kuwaita wakaguzi wa majengo waangalie mafundi wake walivyojenga ili kuepuka hasara anayoweza kuipata,” alisema mtaalam huyo.”
ACHAMBUA UJENZI ULIVYO
“Kuna kitu katika ujenzi tunaita ratio (uwiano) kati ya mchanga wa kujengea na simenti. Huu mchanganyiko inabidi ukamilike kutegemea urefu, unene na ukubwa wa kinachojengwa, kitu chochote kikipungua, matokeo yake ndiyo haya, mafuriko kidogo au tetemeko dogo tu linaweza kuporomosha jumba zima,” alisema Injinia Daniel.
Muonekano wa ukuta huo uliobomoka.
WALICHOSEMA WANAOMJUA DIAMOND
Amani pia lilizungumza na baadhi ya watu wa karibu wa Diamond ambao walisema kuwa, tatizo lililomtokea staa huyo linatokana na tabia ya umaarufu.“Unajua watu maarufu na wenye pesa, wanapojenga wanapenda sana kuwasiliana na mafundi wao kwa njia ya simu. Utakuta mtu yupo mjini, anawasiliana na fundi yupo saiti, fundi anaomba shilingi laki moja anunulie simenti, inatumwa kwa njia ya mitandao ya pesa.
“Sasa hapo unategemea nini? Fundi atatumia elfu hamsini, elfu hamsini ataweka ndani. Ndiyo maana ukiangalia ukuta wa nyumba ya Diamond ulioanguka, nondo zilikuwa nyembamba sana na inaonekana hata simenti ilikuwa chache kwenye matofali,” alisema mmoja wa watu hao akiomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Mwingine alisema: “Ki ukweli Diamond ‘amepigwa’ na mafundi kwenye ile nyumba. Iko haja ya kuchukua wataalam wa majengo wakakague ili kama ni kweli mpaka matofali yaliyotumika kujengea nyumba kubwa yako chini ya kiwango, achukue hatua. Lakini mwenyewe anakimbilia kusema mafundi ni wawili tofauti.”
DIAMOND AULIZWA, AKIRI KUCHAKACHULIWA
Baada ya maelezo hayo yote, Amani liliwasiliana na  Diamond na kumuuliza kuhusu zengwe hilo linalodaiwa amepigwa kwenye mjengo wake aliohamia hivi karibuni.Kwanza alikiri suala la mafundi waliojenga awali kufanya uchakachuaji wa kutumia simenti kiduchu na nondo zisizositahili.
“Ni kweli, wale mafundi nimeambiwa kwa jinsi walivyojenga, walichakachua simenti. Hata hivyo, kwa kulitambua hilo nimechukua mafundi wapya na kazi inayorudiwa sasa ni ya uhakika zaidi. Huu ujanjaujanja uliofanyika hata mimi sijakubaliana nao.”
Amani: “Kwa hiyo unarudia ujenzi wa nyumba yote?”
Diamond: “Aaa! No! Unajua mafundi waliojenga ule ukuta ulioanguka siyo waliojenga nyumba kubwa. Ni mafundi wawili tofauti. Kwa hiyo nina imani nyumba kubwa ipo sawasawa.”
Amani: “Baadhi ya marafiki zako wanasema fundi ni mmoja ila unasema ni wawili ili usibanwe kuhusu kuirudia nyumba kubwa.”
Diamond: “Hamna bwana! Waliojenga ukuta wa uzio siyo wa nyumba kubwa. Ndiyo maana nimewaita wengine kujenja upya uzio. Unajua naishi kwa wasiwasi, maana kama wale walichakachua si ipo siku unaweza kukuta ukuta wote chini na wezi wameingia, nakuwa na wasiwasi sana.”
INJINIA ARUDIWA
Baada ya Diamond kuzungumza hayo kuhusu mafundi wa nyumba kubwa kuwa wengine na mafundi wa uzio, Amani lilimrudia Injinia Daniel na kumuuliza kuhusu sheria ya ujenzi wa aina hiyo inasemaje.“Hapo sasa ni ujenzi holela! Mjenzi anatakiwa kuwa mmoja tu. Huyohuyo wa nyumba kubwa anatakiwa amalizie na uzio kama mtu ataamua kuweka uzio.
Nyota wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond’.
“Ndiyo maana huwa tunawataka watu wafuate sheria za kuajiri wajenzi wenye viwango vya kisheria ili waweke na ule ubao wa maelekezo ya ujenzi.“Kwa kawaida kile kibao kina maelezo ya; project (mradi), contractor (mjenzi), client (mteja), consultant (mshauri), supervisor (msimamizi). Kuna mabango mengine hadi mtoa pesa ambaye ni financier anaandikwa pia na siku ya kuanza ujenzi na makadirio ya kumaliza.”
MAZITO YAIBUKA KUHUSU MJENGO WA KIFAHARI WA DIAMOND MAZITO YAIBUKA KUHUSU MJENGO WA KIFAHARI WA DIAMOND Reviewed by Linnah Lsquare on 12:53 AM Rating: 5
Powered by Blogger.