HATARI SANAAA......Harusi ya Messi Kuonyeshwa Dunia Nzima,Yapangw Kufanyanywa Mara Mbili

Kwa mazingira yetu ambayo hatujazoea, ikitokea mwanamke au msichana anaingia na mtoto uwanjani, kila mmoja atashangaa. Mshangao wenyewe utakuwaje, kwa vyovyote mtoto atakuwa analia.
Pengine hafahamu mazingira yale. Kumbe mama kamleta mtoto kwa kuwa mchezaji fulani kazaa naye, halafu kamsusa, sasa anachotaka kufanya ni kumsusia mtoto uwanjani. Wapo wenye mawazo hayo japokuwa haijatokea lakini matukio ya wanawake kususia wanaume watoto yamewahi kutokea mara kadhaa.
Kwa wenzetu ni tofauti. Hata wapenzi wakitengana, heshima inabakia huko huko.
Nzuri zaidi ni pale mama anapokuja na mtoto au watoto kisha kupiga picha na mwenza wake ambaye ni mchezaji.
Tumeshaona kwa wenzetu wachezaji wakibeba watoto wanaingia uwanjani baada ya mechi wanapiga picha na wenza wao. Sasa, hebu tuchukue mfano huo kwa hapa kwetu, si itakuwa ugomvi kila siku.
Kwanza kuna maeneo maalumu wanatengewa wake za wachezaji, hapa kwetu ikitokea hivyo, wakatengewa, wapo watakaokuwa na staha zao lakini kwa wachezaji vicheche, sijui itakuwaje.

Lionel Messi na Antonella
Lionel Messi amepiga sana picha na mpenzi wake hasa baada ya mechi, walipopata mtoto kisha watoto waliendelea hivyo, na leo hii wanapanga kufunga bonge la harusi, itakayofanyika siku ya kuzaliwa Messi, Juni 24, 2017 siku ambayo atakuwa anatimiza miaka 30.
Wawili hao wamepanga kufanya harusi yao nchini Argentina; katika Kanisa la Basilica Shrine of Our Lady Del Rosario ikiwa ni katika mji aliozaliwa na sherehe nyingine imepangwa kufanyika kitongoji cha Arroyo Seco, Hispania ambako ndiko Messi anakoishi.
Harusi hiyo inafungwa Rosario, ambako pia ndiko walikokutana kwa mara ya kwanza. Messi akiwa bado yanki, alikuwa akienda kucheza mtaa ambao Antonella alikuwa akiishi na mpwa wake, Lucas Scaglia.
Wamepanga harusi yao kuwa ya aina yake, na wamealika watu zaidi ya 700, wakiwemo wanasoka kutoka kila pembe za dunia, waandishi wa habari, marafiki na wanafamilia wa Messi na Antonella.
Lionel na Antonella walioishi pamoja kupika na kupakua tangu 2010 nchini Hispania, wana watoto wawili, Thiago na Mateo.

Harusi funga kazi
Antonella amemwambia Messi kuwa anataka harusi ya mfano, harusi funga kazi ambayo haijawahi kutokea.
Kwa mujibu wa Jarida la Primicias Ya, wawili hao wameanza kufanyia kazi jambo hilo kuhakikisha inakuwa harusi kubwa. Kitu kikubwa ni kwamba wameshafahamu kuwa itafungwa lini na wapi, kwamba mji alikozaliwa wa Rosario ndiko harusi itafungwa.
Hiyo ina maana ya kwamba, harusi itafungwa mahali ambako watu watajirusha kwa kula na kunywa huko Argentina.

Mnuso mwingine Hispania
Kwa mujibu wa televisheni ya mji wa Catalan katika kipindi chake cha Arucitys de la cadena 8TV, baada ya harusi hiyo nchini Argentina, maharusi watahamia Hispania kufanya mambo mengine kwa marafiki zake watakaoshindwa kwenda Argentina ambako ni umbali wa maili 6,500 kutoka Hispania.
Messi ana marafiki wengi na wako vizuri, haitarajiwi kama watashindwa kwenda Argentina kushuhudia akichukua jiko lake, na hata mwenyewe anasema kuwa anataraji marafiki wengi kufika kwenye shughuli yake.
Marafiki zake wakubwa ni pamoja na wachezaji wenzake ambao wengi wameshathibitisha kuwa watakwenda Rosario.
Kitu cha kufurahisha zaidi, waandaazi wa misosi kwa shughuli zote za Argentina na Hispania, watatoka kwenye mji wa Catalan, Hispania na watasafirishwa kwenda Argentina kwa ajili ya kuhudumia vyakula na vinywaji.
Kampuni hiyo ndiyo ilitoa huduma hiyo kwenye harusi ya mchezaji mwingine wa Barcelona, Carles Puyol mwaka 2014.

Kinachosikitisha
Kitu cha kusikitisha ni kwamba, rafiki yake mkubwa Messi, Gerard Pique hatahudhuria harusi hiyo ya mshkaji wake huyo.
Hiyo ni kwa kuwa mpenzi wa Pique, Shakira na mchumba wa Messi, Antonella hawaivi.
Sababu kubwa ni kwamba Antonella alikuwa rafiki wa mpenzi wa zamani wa Pique, Nuria Tomas, sasa inawezekana Shakira anahisi Antonella anafanya ukuwadi kwa jamaa yake, Pique.
Pique na Messi ni marafiki, lakini hasira za Shakira kwa Antonella, inabidi awe mpole tu na wafanye mambo mengine wakati washkaji wengine kwenye timu wakiwa kwenye mnuso.
Pique na Shakira walikutana wakati Nuria bado akiwa mpenzi wa Pique lakini mapenzi motomoto ya Pique na Shakira yalinoga wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2010.
Katika mahojiano na TV3 Oktoba mwaka jana, Pique alisema: “Nimekutana na Shakira mjini Madrid wakati tunajiandaa na Fainali za Kombe la Dunia 2010 baada ya kumwona kwenye video yake ya Waka Waka.

Messi kuaga kwa harusi?
Harusi ya Messi inafungwa wakati ligi mbalimbali zimemalizika, wachezaji wakiwa katika mapumziko na wakati huo dirisha kubwa la usajili litakuwa wazi.
Haijathibitishwa lakini huenda Messi akatumia harusi hiyo kuaga wachezaji wenzake, mashabiki na viongozi wa Barcelona kwa kuwa kuna tetesi anataka kumfuata kocha wake wa zamani, Pep Guardiola ambaye kwa sasa anainoa Manchester City.
Guardiola anamhusudu Messi kupita kiasi kwa kuwa alimbeba kipindi alipokuwa akiinoa Barcelona, alimpa heshima ya mataji kwa kufunga mabao katika mechi muhimu.
Pamoja na hayo, inaelezwa kuwa Messi hakukurupuka kusema kuwa anatakiwa na Manchester City, aliuambia uongozi wa juu wa Barcelona kilichopo mbele yake na azma ya Guardiola kwake.

Messi na Antonella walianzaje?
Mara nyingi, mtu yeyote hata wachezaji, wanakuwa hawana kitu, sasa wanapopata maisha mazuri, wanasahau walikotoka, wanataka vizuri vipya, lakini hiyo ni tofauti kwa Messi.
Messi ana pesa za kutosha, ana utajiri lakini hakumsahau mtu wake walioanza naye siku nyingi.
Unajua walianzia wapi? Baba yake Antonella alikuwa anamiliki duka kubwa la mahitaji mbalimbali na vyakula, supermarket mtaani kwao walipokuwa wanaishi.
Malavidavi yao hasa (Messi na Antonella) yalianza mwaka 1996, wakati Messi akiwa mdogo tu wa miaka tisa.
Rafiki mkubwa wa Messi hapo mtaani kwao alikuwa mpwa wake, Antonella, Lucas Scaglia, walikuwa wakicheza pamoja na pia walikuwa pamoja kwa mambo mengi ikiwamo kuwa katika shule moja iliyokuwa inaitwa Newell’s Old Boys, katika mji wa Rosario.
Mara nyingi, Messi alikuwa akiaga nyumbani anakwenda kwa akina Scaglia kwa kuwa naye alikuwa akifahamika nyumbani kwao.
Wakati mwingine walikuwa wanakwenda kutembea pwani ya Mto Parana. Messi pamoja na kwamba alikuwa dogo wa miaka tisa, lakini alikuwa kamzimia Antonella.
Iliendelea hivyo na walizoeana vizuri kwa kuwa Antonella alipenda kwenda nao (Messi na Scaglia) wakiwa katika matembezi kama hayo ya ‘beach’ na walirudi nyumbani.
Wakiwa beach pamoja na kuwa wanapiga stori za kawaida za mtaani na hata mazingira ya beach na mengine, kumbe moyo wa Messi ulishamdondokea Antonella siku nyingi lakini Antonella hajui kitu.
Kwa kuwa walikuwa na mambo ya kitoto, Messi alikuwa na tabia ya kumwandikia Antonella barua za mapenzi, akimwambia angetamani siku moja awe mpenzi wake. Mambo yale ya enzi za shule.
Kama unavyojua, wenyewe walielewana lakini kwa kificho, walikuwa wapenzi wa sirisiri hadi Messi alipotimiza miaka 21, ikaja kufahamika kuwa kumbe Messi alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Antonella.
Mapenzi siku zote hayafichiki, hayana siri, kipindi cha televisheni cha ‘Hat Trick Barça’, iliyoko kwenye mji wa Catalan channel ‘TV3’, kiliweka wazi hayo na hiyo ilikuwa Januari 2009.
Siku moja Messi alikuwa akihojiwa, si unajua inapofika wakati wa maswali ya kizushi, akaulizwa, “Una rafiki wa kike?” Na Messi akajibu “Ndio, ninaye rafiki. Yuko Argentina. Ukweli ni kwamba yuko vizuri na sina presha naye.”
Si unajua wadaku, wakamwambia wamesikia Messi amekutaja, na Antonella naye alikuwa akifuatilia kila anachofanya Messi na kila kinachoandikwa kuhusu Messi.
Baada ya kuelezwa alichosema Messi, akaanza sasa kuonyesha malavidavi na mawasiliano kila siku, ‘I miss u’ nyingi zikaanza kwa kuwa alijihakikishia kuanzia hapo.
Antonella, alikuwa akisoma Latin American Education Centre, na hata hivyo haikumchanganya sana, kwani akiwa na miaka 13, Leo alikwenda Barça kwenye Mji wa Catalan.
Kipindi Messi anaanza kuwa staa wa dunia na anasikika kila kona, Antonella wakati huo alikuwa na ‘mchepuko’ mmoja naye alikuwa akiishi kwenye mji huo wa Rosario, ni jirani tu na kwao, lakini mapenzi yao yalidumu kwa miaka mitatu.
Baada ya kimya cha muda, siku moja mtaani kwao hapo palitokea msiba, rafiki mkubwa wa Antonella alifariki kwa ajali na Messi alisikia akapanda ndege na kuhudhuria msiba ule, akitokea Hispania, hapo wakakutana tena na Antonella. Kuanzia kwenye msiba ule na hadi leo mambo ni bambam hadi harusi.
Jarida la ‘Infobae’, linasema kuwa Messi amekuwa akisafiri ‘fasta’ anaposikia kuna jambo limetokea mtaani kwao huko Argentina na wakati wote anakuwa karibu mno na Antonella.
Hapo kabla, unaambiwa mapenzi ndiyo kama hivyo, yalikuwa ya sirisiri lakini baadaye wakaja kuyaweka hadharani, kuwa Messi na Antonella ndio vile tena.
Baada ya maziko ya rafiki wa Antonella, Messi alirudi Barcelona, wakati huo Antonella naye alianza kusoma masuala ya Odontology yaani alitaka kuwa mtaalamu wa mfumo wa fizi na meno na magonjwa yake katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Rosario.
Hata hivyo, aliona mambo magumu, akabadilisha kozi baada ya miezi sita, akaanza kusoma mawasiliano ya jamii, aliyosoma kwa mwaka mmoja.
Marafiki wa Antonella walisema kuwa rafiki yao alikuwa akiwaringishia kuwa yuko katika mahaba na Messi na hiyo ilikuwa Julai 20, 2007. Mapenzi yao yalizidi kunoga zaidi wakati wa Fainali za Kombe la Dunia 2010 zilizofanyika Afrika Kusini.
Baada ya fainali zile za Afrika Kusini, Messi aliamua kumbeba Antonella na kwenda naye Barcelona kwa mara ya kwanza.
Juni 2, 2012, baada ya Messi kufunga bao katika mechi dhidi ya Ecuador kwenye Uwanja wa Monumental, alifuatiliwa na siri ikafichuka kuwa Antonella alikuwa na ujauzito na mtoto aliyezaliwa alipewa jina la Thiago, mtoto huyo alizaliwa Novemba 2, 2012.
Msimu wa Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga wa 2014/15, Messi aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa Antonella anataraji kupata mtoto wa pili, atakayeitwa Mateo, huyu naye alizaliwa Septemba 11, 2015.
Huu ni ushahidi tosha kuwa maisha ya Messi na Antonella yanastahiki kuandikiwa hadithi nzuri ya mapenzi.
Messi anajua kuwa anapendwa, na Antonella anaonyesha mapenzi ya dhati kuwa anampenda au ana mapenzi ya kweli na Messi na sasa kitu pekee kilichobaki ni Juni 24, 2017.
HATARI SANAAA......Harusi ya Messi Kuonyeshwa Dunia Nzima,Yapangw Kufanyanywa Mara Mbili HATARI SANAAA......Harusi ya Messi Kuonyeshwa Dunia Nzima,Yapangw Kufanyanywa Mara Mbili Reviewed by Linnah Lsquare on 1:53 AM Rating: 5
Powered by Blogger.